Leo ni siku ya Saratani Duniani. Wakati tunaadhimisha siku hii
hapa nchini idadi ya vijana ambao ni tegemeo la taifa inazidi kupungua
kutokana kuangamia kwa saratani ikiwemo ya koo.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani
(WHO) nchini umeonyesha asilimia 20 ya saratani ya koo husababishwa na
ngono ya mdomo maarufu kama ‘Oral Sex”.
Utafiti huo unaonyesha saratani ya koo licha ya kuambukizwa na njia mbalimbali ikiwemo ulaji wa vyakula vyenye pilipili,
pombe kali, vitu vyenye uchachu pamoja na kurithi kutoka kwa wazazi.
Utafiti unaonyesha watu wengi hasa vijana
wanamejiingiza kwenye vitendo hivi vya kufanya ngono wakitumia midomo
hasa ndimi, hivyo kuhatarisha uhai wao.
Katika utafiti huo wa hivi karibuni, ulibaini
wanaume 747 na wanawake wakiwa 472 hugundulika kila mwaka kuwa na
saratani hiyo huku wanaopoteza maisha kila mwaka ni wanaume 444
wakifuatiwa na wanawake 270 kutokana na ugonjwa huo.
Utafiti unabainisha kuwa asilimia kubwa ya vijana
wenye umri kati ya miaka 20 hadi 45 wanatumia staili ya kuwanyonya wenza
wao sehemu za siri lengo likiwa ni kuwavutia wapenzi wao katika
kushiriki ngono.
Vijana wenye umri huo ndio wahanga wakubwa kwa
sasa kutokana na ugonjwa huo kuonekana kuwaathiri kwa kasi, huku wengi
wakiwa hawajui athari zake. Baadhi hujisifia kwamba ni wajuzi, kumbe
wanajitafutia kifo kwa kufanya vitendo hivyo.
Utafiti unaonyesha kwa watu wazima walio wengi
hawana muda wa kufanya hayo wanayofanya vijana, hivyo kujikuta angalau
wanakuwa salama na kupatwa na saratani ya koo kwa njia hiyo inayoonekana
kama ni chafu pia.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Crispin Kahesa anasema saratani
ya koo ni ya pili katika mtiririko wa saratani zinazowapata wanaume
nchini, ikiongozwa na ile ya ngozi (Karposi’s Sarcoma) ambayo
huambukizwa kwa njia ya kujamiana. Kuna saratani aina zaidi ya 24
zinazoisumbua Tanzania.
Anasema mbali na staili hiyo pia, kuna baadhi ya
watu hupata saratani ya koo kwa kurithi kutoka kwa wazazi wao na
wengine kuwa na umri mkubwa ambao huchangia kupata tatizo hilo, lakini
siyo kwa asilimia kubwa kama ile ya ngono ya mgomo.
“Hali hii ya vijana wenye umri huo kuwanyonya
wanawake inatokana na ujana, wengine wanaiga kwenye mitandao, lakini
mambo haya hayakuwepo zamani tofauti na sasa, utakuta wanaume ili aweze
kumvutia mwanamke anamfanyia hivyo sehemu za siri, lakini zamani staili
hii haikuwepo kabisa,” anasema Dk Kahesa na kuongeza.
“Kuna njia nyingi tu za kumvutia mwanamke lakini siyo hii bila
kujua madhara yaliyopo, vijana wengi nchini wanaona njia rahisi ya
kupendwa na mwanamke ni hiyo wakati kuna njia nyingi za kufanya. Nje ya
hiyo wanawake wengine huwa na magonjwa mbalimbali, kwa jumla hakuna
usalama wowote kwa wanaume kufanya kitendo hicho,”anaongeza
Sababu nyingine zaidi
Anasema staili ya maisha nayo imechangia
kuongezeka kwa ugonjwa huo, vijana wengi kwa sasa hutumia muda mwingi
kuangalia video za ngono na staili zinazofanywa na wenzetu wa nje na
hivyo kuongezeka kwa matumizi ya ngono ya mdomo.
Dk Kahesa anasema asilimia 12 ya wagonjwa wote wa
saratani nchini wanasumbuliwa na saratani ya koo, hivyo kuna kila
sababu kwa vijana kubadilisha tabia na kuepuka kuiga mitindo ya wenzetu
wazungu ambayo mara nyingi inapotosha mila na tamaduni za Kiafrika.
Anasema katika mtiririko wa saratani zinazoongoza
nchini saratani ya koo inashika nafasi ya tano, wagonjwa wengi
wanaopatwa na ugonjwa huo ni watu wenye umri mkubwa wa miaka 60 na
kuendelea hiyo inaonyesha kuwa wengi wao walianza ngono ya mdomo muda
mrefu wakati wakiwa bado wadogo.
“Asilimia kubwa ya wagonjwa wanaopatikana na kansa
ya koo nchini, inawapata watu wenye umri wa kuanzia miaka 60 na
kuendelea kutokana na wengi wao kuanza mapema vitendo vya ngono kwa
njia ya mdomo wakati bado wadogo au wengine kurithi kutoka kwa wazazi
wao,” anasema Dk Kahesa.
Aina ya kansa ya koo
Tafiti zinaonyesha kuna aina mbili za saratani ya
koo; aina ya kwanza ni “Oesophagus Carcinoma na Squamous cell carcinoma,
zote hutofautiana wakati zinapimwa kwenye darubini lakini matibabu
yake yanafanana.
Aina hizo ndizo zilizopo nchini na huanza mapema
kuharibu seli ambazo zipo katika utandu uliopo katika ukuta wa koo
kabla ya kuenea katika maeneo mengine ya koo.
SOURCE:Hadija Jumanne,Mwananchi

No comments:
Post a Comment